
PAMOJA na kuwa mpaka sasa hakuna mgonjwa mwenye virusi vya homa hatari ya ebola, wala anayehisiwa kuwa na ugonjwa huo nchini, Serikali imeshajiandaa kukabiliana na ugonjwa huo, ambao umeshaua zaidi ya watu 1,000 katika nchi za Afrika Magharibi.
Katika
maandalizi hayo, Serikali imeagiza vituo kadhaa katika mikoa yote, kuwa tayari
kutoa huduma endapo atatokea mgonjwa aliyepata maambukizi ya ugonjwa huo
nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu hatua hizo, Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema katika vituo hivyo vifaa kinga pamoja
na dawa vimeshaandaliwa.
Katika
Mkoa wa Dar es Salaam, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Temeke
Isolation Unit, yametengwa maeneo ya kuhudumia wagonjwa wa ebola endapo
watatambuliwa. Eneo la Temeke bado linaendelea kuboreshwa kwa kuzingatia vigezo
maalumu ili likidhi mahitaji ya matibabu ya ugonjwa huu,” alisema Dk Rashid.
Alisema
wizara hiyo, pia imetoa mwongozo kwa maeneo yaliyoainishwa katika mikoa yote
Tanzania Bara, kuandaa sehemu ya kutenga wagonjwa wakati wa matibabu na
itahakikisha kuwa maeneo hayo
Ingawa
hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya
ebola hapa nchini, lakini hatua hizo zimechukuliwa kwa tahadhari, kwa sababu
kwa mujibu wa Dk Rashid, magonjwa hayatambui mipaka ya nchi.
Akizungumzia
tahadhari hizo, Dk Seif alisema pamoja na kutenga maeneo hayo, pia Serikali
imeunda kikosi kazi kinachohusisha wajumbe mbalimbali wakiwemo wadau wa
maendeleo na watendaji wengine, kwa ajili ya kuandaa kwa kina hatua za dharura
zinazotakiwa kudhibiti ugonjwa huo.
Wadau
hao waliomo katika kikosi kazi hicho ni Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika
la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Msaada la Marekani
(USAID), Shirika la Maendeleo la Kikoloni (CDC) na watendaji wengine kutoka
taasisi za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Kikosi
hiki kimeshakutana mara nne kwa ajili ya kuandaa kwa kina hatua za dharura
zinazotakiwa kuchukuliwa, ili kudhibiti ugonjwa huu usiingie hapa nchini.
Tayari kikosi hiki kimeandaa Mpango wa Dharura wa kukabiliana na ugonjwa wa
ebola kuanzia ngazi ya Taifa hadi wilaya,” alisisitiza.
Alisema
mpango huo unaainisha maeneo mbalimbali, ikiwemo ufuatiliaji wa ugonjwa huo,
namna ya kutambua na kuchukua sampuli, matibabu ya wagonjwa, mwongozo wa namna
ya kutenga sehemu maalumu, uelimishaji wa umma na ushirikishwaji wa wadau
wengine mbalimbali katika kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa ebola.
Dk
Seif pia alisema kikosi kazi hicho kitatumika kutoa tahadhari kwa umma, kuhusu
tishio la ugonjwa huo ambapo tayari tahadhari hiyo ilitolewa Agosti 2, mwaka
huu kupitia vyombo vya habari.
Tahadhari
hiyo ilitolewa Agosti 2, 2014 kupitia vyombo vya habari, ambapo iliainisha
namna ya kutambua ugonjwa huo, umuhimu wa kuwahi matibabu, jinsi ya kujikinga
na pia hatua gani zinatakiwa kutekelezwa na jamii ili kudhibiti ugonjwa hio.
Mipakani
Pamoja na hayo, alisema Serikali katika kuendelea kuchukua tahadhari, pia
imeboresha ufuatiliaji na utambuzi wa ugonjwa huo katika maeneo ya viwanja vya
ndege na mipakani ili kubaini wasafiri watakaoonesha dalili za ugonjwa au wenye
viashiria hatari.
Alisema
fomu maalumu za kuhoji wasafiri, zimeanza kutumika katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na wa Kilimanjaro (KIA) kuanzia Agosti 5,
mwaka huu ambazo pia zitatumika katika maeneo yote ya mipakani.
“Orodha
ya abiria kwenye ndege pia imeanza kutumika, ili kutambua abiria wanaoingia
nchini na kuainisha nchi walizotoka kabla ya ndege kutua nchini,” alisema.
Alisema
Wizara pia imeagiza mashine aina ya “Thermoscanners” zitakazowekwa katika
viwanja vyote vya ndege, kwa ajili ya kurahisisha utambuzi wa wasafiri
watakaokuwa wanaingia nchini na kuwa na dalili za mwanzo ambayo ni homa.
“Wasafiri
wanaoondoka watapewa vipeperushi vya kuelimisha. Katika viwanja hivi, vifaa
kinga vimesambazwa kwa ajili ya watumishi wa afya,” alisisitiza.
Aliwatoa
hofu wananchi kuhusu ugonjwa huo na kuwataka kuendelea kuchukua tahadhari, huku
akisisitiza kuwa ebola inazuilika endapo watu wataepuka kugusa au kuingiwa na
mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi na majimaji mengine yanayotoka
mwilini kwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huo kupitia sehemu zenye michubuko au
vidonda.
Aidha
aliwataka kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za
ugonjwa huo, na badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha huduma za
afya kwa ushauri, ili kuruhusu wataalamu kusimamia maziko ikiwa itatokea.
Dalili
za awali za ugonjwa huo ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya
misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni.
Mara
nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, kutokwa na vipele vya
ngozi, figo na ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa, hutokwa
damu ndani na nje ya mwili.
Ugonjwa
wa ebola hauna tiba maalumu wala chanjo. Hata hivyo mgonjwa anatibiwa kutokana
na dalili atakazokuwa nazo.
Katika
hatua nyingine, vipimo vya watu wawili waliohisiwa kuwa na ugonjwa huo Uganda na
Rwanda, vimebaini kwamba hakuna hata mmoja wao aliyeambukizwa ugonjwa huo.
Waziri
wa Afya wa Rwanda, Agnes Binagwaho alisema jana kuwa mwanafunzi mmoja wa
Ujerumani, aliyefika nchini humo akitokea Liberia, ambayo ni miongoni mwa nchi
nne za Afrika Magharibi ambazo virusi vya ebola vimeenea, alihisiwa kuwa na
ugonjwa huo, lakini baada ya sampuli ya damu yake kupimwa katika maabara za
kimataifa, hakukutwa na ugonjwa huo.
Msemaji wa Wizara ya Afya wa Uganda, Rukia
Nakamatte, naye mwishoni mwa wiki alitoa taarifa kwamba mtu mmoja nchini humo
aliyekuwa amewekwa katika chumba cha pekee baada ya kuwa na homa, baada ya
kupimwa hakukutwa na virusi vya ebola.
No comments:
Post a Comment