BAADA
ya kuwaona magwiji wa Real Madrid wakiongozwa na Luis Figo, sasa mashabiki wa
soka wa Tanzania watakishuhudia kikosi cha sasa cha timu hiyo bingwa wa bara la
Ulaya.
Juzi Jumamosi, Figo akiwa na mwanasoka mwingine
mahiri wa zamani duniani, Fabio Cannavaro, walicheza kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam mbele ya maelfu ya mashabiki. Katika pambano hilo la kimataifa la
kirafiki dhidi ya kikosi cha wakongwe nchini, Tanzania XI, Real Madrid
walishinda mabao 3-1.
Baada
ya kuvutiwa na mchezo huo uliowagusa maelfu ya Watanzania ambao uliratibiwa na
Kampuni ya TSN Supermarkets, Real Madrid ya sasa inaletwa nchini kama magwiji
hao.
Rais
Jakaya Kikwete aliyeshuhudia pambano hilo akitokea safarini kikazi mikoa ya
Morogoro na Arusha, ameweka wazi kuwa mipango ya kuwaleta kina Cristiano
Ronaldo, Gareth Bale, James Rodriguez na wengine imeanza.
“Watanzania
wamefurahishwa sana na kuja kwenu pamoja na pambano safi walililoona jioni ya
leo (juzi) pale uwanjani.
“Sasa
tunataka ije timu ya sasa ya Real Madrid. Nimezungumza na Balozi (wa Hispania
nchini), atasimamia jukumu hilo,” alisema Rais Kikwete, juzi usiku Ikulu katika
chakula cha usiku alichokiandaa kwa timu hizo mbili.
Balozi
wa Hispania nchini, Luis Manuel Civis, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria hafla
hiyo.
Rais
Kikwete ambaye chini ya utawala wake, amekuwa mstari wa mbele kusaidia sekta ya
michezo, alisema mashabiki wa soka na Watanzania kwa ujumla waliojitokeza
Taifa, wamefurahishwa sana na pambano hilo la juzi.
Aidha,
Rais Kikwete alisema ushirikiano kati ya Tanzania na Real Madrid utaendelezwa
zaidi kwa kuhakikisha miamba hiyo inajenga kituo chake cha mafunzo ya soka kwa
vijana.
Magwiji
hao wa zamani mbali ya kupata fursa ya kula chakula na Rais Kikwete na viongozi
wengine wa Serikali, pia Rais aliwapa kila mmoja zawadi ya kinyago cha
Kimakonde.</p>
Awali,
Figo na wenzake akiwamo nahodha wa Italia aliyetwaa Kombe la Dunia 2006, Fabio
Cannavaro walimkabidhi Rais jezi iliyosainiwa na wachezaji wa timu hiyo bingwa
wa Ulaya.
Aidha,
wachezaji hao walimpatia pia jezi kama hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TSN
Supermarkets, Farough Baghozah, ambaye amefanikisha ziara hiyo ya kwanza ya
aina yake kwa miamba hiyo Tanzania na barani Afrika.
Magwiji
hao wa Real Madrid jana walitarajiwa kutembelea mlima Kilimanjaro mjini Moshi
na leo watakuwa Arusha kutembelea kreta ya Ngorongoro kabla ya kurejea makwao
kesho.
No comments:
Post a Comment