
SERIKALI
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imebaini kuwepo kwa mlipuko wa
maradhi ya homa kali maeneo ya Kaskazini mwa nchi hiyo, ambayo sasa
imethibitika kuwa ni ugonjwa wa ebola.
Waziri
wa Afya wa nchi hiyo, Dk Felix Numbi, aliliambia Shirika la Utangazaji la
Uingereza (BBC) jana, kwamba watu wawili wamepimwa na kugundulika wanaumwa
ebola, maradhi ambayo hadi sasa yameshaua watu 13 katika jimbo la Equateur.
Lakini,
maradhi hayo yako maeneo ya vijijini na imeelezwa kuwa ebola hiyo, ni tofauti
na ile inayosumbua nchi za Afrika Magharibi. Shirika la Afya Duniani (WHO)
limekiri kuwa mlipuko wa ebola kwa sasa hautarajiwi kuwa na kasi kubwa katika
nchi za Afrika Magharibi, ambako tayari watu 2,615 wameshakumbwa na maradhi
hayo tangu ulipuke Machi mwaka huu.
Hadi
sasa maradhi hayo hayana tiba, lakini baadhi ya wagonjwa wamepona baada ya kupewa
dawa aina ya ZMapp, ambayo bado iko kwenye majaribio.
Hata
hivyo, dawa hizo zimemalizika na hazipo tena. Dk Numbi alisema watatangaza
karantini ya watu kuingia na kutoka katika mji wa Boende, ambako wagonjwa wa
homa hiyo wamegundulika.
Mji huo upo kilometa 100 kutoka jiji la
Kinshasa. Alisema kuibuka tena kwa mlipuko huo, kumesababisha idadi ya milipuko
ya homa ya ebola kufikia saba tangu 1976 mgonjwa wa kwanza alipogundulika karibu
na Mto Ebola.
Akizungumza
na gazeti hili jana kuhusu tishio la ugonjwa huo katika nchi jirani na
Tanzania, Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
anayeshughulikia Dharura na Maafa, Dk Elias Kwesi, alisema Serikali imeendelea
kuimarisha ulinzi na usalama mipakani na katika viwanja vya ndege.
Dk Kwesi alisema ulinzi huo, umeenda sambamba
na upimaji wa afya za watu wanaoingia nchini, ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Alisema mpaka sasa hakuna taarifa rasmi kutoka WHO za kuwepo kwa ugonjwa huo
nchini Kongo.
Dk Kwesi alisema mpaka sasa tayari
wameshafunga vifaa vya kisasa katika viwanja vyote vya ndege.
Mpango
uliopo ni kufunga vifaa vingine katika mipaka yote na tayari utekelezaji wa
mpango huo, umeshaanza katika mpaka wa Namanga.
Kwa
mujibu wa Dk Kwesi, wiki hii wanatarajia vifaa vingine vya upimaji kuwasili na
vitasambazwa katika mipaka ya Holili, Sirari na Mtukula.
Lengo
ni kuhakikisha mipaka yote imefungwa vifaa hivyo, ili watu wanaoingia kupitia
mipaka hiyo, wapimwe afya zao kwanza.
Alisema tayari wameshatoa mafunzo kwa
wataalamu wa afya wa mikoa mbalimbali, ikiwemo mikoa ya pembezoni ambayo nao
wanatakiwa kufundisha wahudumu wa afya na jamii dalili za ugonjwa huo na namna
ya kukabiliana nao. Dalili zake ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu
ya misuli, kuuma kichwa na vidonda kooni.
Mara
nyingi dalili hizo hufuatiwa na kutapika, kuharisha, vipele vya ngozi, figo na
ini kushindwa kufanya kazi na kwa baadhi ya wagonjwa kutokwa damu ndani na nje
mwilini. Muda wa kuonekana kwa dalili za ugonjwa huo ni kati ya siku mbili hadi
21 baada ya kupata maambukizi.
“Ugonjwa
wa ebola unaambukiza kwa kasi na unaenea kati ya mtu na mtu kwa kugusa damu na
majimaji kutoka mwilini mwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa huo, kugusa maiti ya mtu
aliyekufa kwa ugonjwa huo na kugusa wanyama walioambukizwa mizoga na wazima
kama vile sokwe na swala wa msituni,” imeeleza taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa
hivi karibuni.
Katika
hatua nyingine, baada ya ugonjwa huo kuua madaktari na wataalamu wa maabara,
Taasisi ya Kupambana na Magonjwa Ambukizi Kusini mwa Jangwa la Sahara (SACIDS),
imeamua kutoa mafunzo kwa wataalamu hao, ili kusaidia waepukane na hatari ya
kuambukizwa magonjwa hayo.
Wataalamu
na wanafunzi hao 45 kutoka katika ukanda huo, ikiwemo, Kenya, Uganda, Kongo
DRC, Zambia, Msumbiji, Afrika Kusini na mwenyeji Tanzania, walikutana mkoani
Morogoro kujadili umuhimu wa kuongeza usalama katika kuhifadhi sampuli za
ugonjwa huo ili zisisambae.
Mkurugenzi
wa taasisi hiyo, Profesa Mark Rweyemamu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha
Sokoine (SUA), alisema wameamua kuchukua wataalamu na wanafunzi kutoka katika
nchi hizo, ili wapate elimu ya jinsi ya kujikinga, ikiwa kutatokea mlipuko wowote
wa ugonjwa huo.
Alisema
kuwa asilimia 20 ya watu katoka katika ukanda huo, hufariki dunia kwa magonjwa
ya kuambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa bindamu.
Mhadhiri
wa SUA, Esron Karimuribo, alisema Bara la Afrika limekuwa likikumbwa na
magonjwa mengi ambukizi, ikiwemo ebola na magonjwa mengine yanayofanana na hayo.
Alisema
kuwa ushirikiano kati ya sekta ya afya na mifugo, ni muhimu kwa kuwa magonjwa
mengi yanayowapata binadamu yanatokana na mifugo.
Mkuu
wa Idara ya Maikrobayolojia na Parasitolijia katika Kitivo cha Mifugo cha SUA,
Gerald Misinzo, alitoa mfano wa homa ya bonde la ufa, kuwa huathiri wanyama na
binadamu.
Mkurugenzi
wa Sayansi ya Uhai Tanzania, Flora Ismail, alisema bioteknolojia inatoa suluhu
kinzani za magonjwa, ikiwa ni pamoja na kuzalisha chanjo ya magonjwa mbali
mbali yanayosababishwa na wanyama na katika kilimo wamepata suluhu kwa kuchagua
mbegu bora.
Imeandikwa
na Shadrack Sagati, Hellen Mlacky, Dar, Agnes Haule, Morogoro na mashirika ya
habari.
Source:Habari Leo
No comments:
Post a Comment