
USAJILI wa straika Emmanuel Okwi ndani ya Simba, umemshtua kocha Patrick Phiri ambaye amesema haelewi nini kimetokea na sasa amewaachia viongozi waamue nani anafaa kuachwa ama kuendelea.
Juzi Alhamis jioni
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe, alimtangaza rasmi Okwi
kuwa mchezaji mpya wa Simba kwa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.
Mpaka jana Ijumaa
mchana Okwi alikuwa hajajiunga na kambi hiyo iliyopo visiwani hapa huku
kukiwepo taarifa kuwa angewasili muda wowote na taarifa za ndani zilisema kuwa
beki Mkenya Donald Mosoti ndiye aliyekuwa kwenye mpango wa kuachwa.
Simba ilipitisha
majina ya wachezaji 28 wakiwemo wachezaji watano wa kigeni ambao ni
washambuliaji Amissi Tambwe, Raphael Kiongera, Pierre Kwizera, Joseph Owino na
Mosoti.
“Bado nipo gizani,
nimesikia taarifa hizo lakini nasubiri taarifa ya viongozi, naamini uongozi wa
Simba upo vizuri katika kusajili hivyo mchezaji nitakayeletewa atakuwa mzuri
maana wao wamemuona na amewahi kuichezea Simba,” alisema Phiri.
“Soka la Tanzania
ni kama siasa hivyo tunatakiwa kukubaliana na hali halisi, mimi ni mtaalamu wa
benchi la ufundi lakini viongozi pia wana utaalamu wao, hivyo naamini usajili
wao utakuwa mzuri.”
Kuhusu taarifa za
kutemwa kati ya wachezaji wake Mosoti au Tambwe, Phiri alisema: “Mosoti sikumpa
nafasi sana ya kucheza mechi hizo kwa sababu wengi wanamfahamu na Butoyi
Hussein amekuja kwa ajili ya majaribio hivyo ilikuwa ni lazima apewe nafasi ili
aonyeshe kiwango chake.
“Tambwe ni mchezaji
mzuri na ndiye mfungaji bora wa ligi msimu uliopita, binafsi alicheza vizuri
pamoja na Said Ndemla katika mechi zilizopita, nikiwa kama kocha siwezi kusema
mchezaji ameshuka kiwango kwa mechi za kirafiki.”
No comments:
Post a Comment