Sunday, August 31, 2014

MUAFAKA WA KATIBA MPYA SASA WANUKIA


MKUTANO wa Rais Jakaya Kikwete na viongozi wa juu wa vyama vya siasa uliofanyika jana mjini Dodoma umetajwa kuwa na dalili nzuri zinazoashiria mwafaka utapatikana juu ya mchakato wa utengenezaji
Katiba mpya. Kikwete alikutana jana na vyama hivyo kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kinachoongozwa na Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo kukiwa na ajenda mbili mojawapo ikihusu mchakato unaoendelea wa kutengeneza Katiba mpya.
TCD inaundwa na vyama vyenye uwakilishi bungeni, ambavyo ni CCM, CUF, CHADEMA, TLP, NCCR-Mageuzi na UDP. Ingawa
yaliyojiri ndani ya mkutano huo unaotajwa ulijaa amani na ucheshi hayakuwekwa wazi, Cheyo ambaye ni Mwenyekiti wa TCD alisema ajenda nyingine ilihusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Cheyo alisema mkutano huo ulienda vizuri na wamekubaliana Septemba 8, mwaka huu, kukutana kwa mazungumzo zaidi ambayo anaamini kutakuwa na matokeo chanya.
“Mkutano umeenda vizuri sana…ulikuwa mkutano mzuri sana, ulijaa amani na ucheshi. Tumekubaliana kwamba tunakutana tarehe 8, Septemba,” alisema Cheyo.
Akielezea imani yake juu ya mkutano huo wa wiki ijayo katika suala zima la kupata mwafaka juu ya mchakato wa Katiba mpya, baada ya Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususa, Cheyo alisema, “…kukubaliana kukutana tu, ni jambo muhimu sana na lenye dalili nzuri.”
Kwa mujibu wa Cheyo, mkutano huo ulitawaliwa na utulivu, ucheshi jambo ambalo anaamini utamaduni wa Watanzania wa kukaa na kuzungumza utazaa matunda katika mkutano ujao.
Cheyo ambaye alishiriki pamoja na Katibu wa chama chake, Isack Cheyo, alisema wanachama wote wa TCD akiwemo mwakilishi wa vyama visivyo na wabunge, walihudhuria na kushiriki mkutano huo kwa ufasaha.
Kwa upande wa CCM, walioshiriki ni Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana. Chadema aliyeshiriki ni Katibu Mkuu wake, Dk Wilbrod Slaa pamoja na Mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu.
Washiriki wengine ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia na Katibu Mkuu wake, Mosena Nyambabe.
CUF iliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya.
Kwa upande wa TLP, Mwenyekiti wake, Augustino Mrema na Katibu Mkuu wake, Jeremiah Shelukindo walishiriki.
Aidha Mwenyekiti wa United Peoples Democratic Party (UPDP), Fahmi Dovutwa aliwakilisha vyama visivyo na wabunge katika
TCD. Cheyo alisema kabla ya mkutano huo wa wiki ijayo, Septemba 6 na 7, TCD itakuwa na mkutano wake mkuu utakaokutanisha wanachama kabla ya kesho yake kukutana na Rais.
Ajenda kuhusu mchakato wa Katiba mpya, unazingatia hali ya sasa ya kisiasa ambayo, kundi la Ukawa lilisusa Bunge Maalumu la Katiba kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wake.
Tangu Ukawa wasuse Bunge hilo linaloendelea mjini Dodoma, wananchi na makundi mbalimbali ya kijamii yamekuwa yakitaka wajumbe hao waliosusa warejee bungeni kuungana na wenzao waliobaki kutengeneza Katiba yenye maridhiano.
Licha ya kuwepo sauti za kusihi kundi hilo kurejea bungeni, pia wapo ambao wamekuwa wakisisitiza maridhiano kati ya Ukawana Tanzania Kwanza yapatikane ili kuunda Katiba yenye ushiriki wa makundi yote.
Wadau wengine, likiwemo Jukwaa la Wakristo Tanzania lililotoa taarifa yake jana kuhusu mchakato wa Katiba, na kumwomba
Rais Kikwete asitishe Bunge hilo ili upatikane mwafaka na maridhiano.Katika taarifa ya jukwaa hilo linalojumuisha Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Baraza la Makanisa ya Pentekoste (CPCT),
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Kanisa la Waadventista Wasabato, limeomba mchakato uahirishwe kuepusha athari kwa mshikamano na umoja wa taifa.
Mjadala bungeni kesho BUNGE Maalumu la Katiba litaanza majadiliano kesho baada kamati zote kumaliza kupitia na kuchambua sura zote za Rasimu ya Katiba. Jana na leo kwa mujibu wa Katibu wa Bunge hilo, Yahya Hamad kamati hizo ilikuwa ziwasilishe taarifa zao kwa Sekretarieti ya Bunge ambayo itaanza kuzichambua kabla ya kuzipeleka kwenye Bunge.
Hamad alisema licha ya kuzichambua, Kamati ya Uongozi itakutana leo kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali kabla ya majadiliano kuanza kesho.
"Ratiba yetu inaonesha kuwa Jumanne (kesho) Bunge lote litakutana kwa ajili ya majadiliano ambayo ni muhimu sana ili kuwekana sawa," alisema Hamad. Alisema siku 15 zimepangwa kwa ajili ya majadiliano ili taarifa hizo pamoja na maoni ya wajumbe wakati wa mjadala yawasilishwe kwa Kamati ya Uandishi wa Rasimu ya Katiba.
Hamad alisema Bunge hilo likishakamilisha mjadala, ndipo Kamati ya Uandishi wa Katiba ambayo iko chini ya Mwanasheria maarufu Andrew Chenge itaanza kazi ya kuandika Rasimu ya Katiba.
Alisema Kamati ya Chenge pia italazimika kurejesha Rasimu hiyo ndani ya Bunge kuona kile walichokiandika ni sahihi kabla ya kupigiwa kura na wajumbe wote. Bunge hilo limehitimisha siku 30 ambazo walizitumia kwa kamati mbalimbali kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa bungeni hapo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Kwenye majadiliano hayo, kamati mbalimbali zilitupilia mbali baadhi ya mapendekezo yaliyoko kwenye Rasimu ya Katiba ikiwemo lile linalotaka wabunge wawe na ukomo na wananchi kupewa haki ya kumwondoa mbunge wao madarakani.
Eneo lingine ambalo baadhi ya kamati ziliyakataa ni ambayo yalitaka baadhi ya wateule wa Rais kutakiwa kuthibitishwa na Bunge kwa maelezo kuwa viongozi wanaotakiwa kuthibitishwa na chombo hicho, ni wale tu wanaowajibika kwa Bunge hilo.
Lakini pia kuna mvutano wa aina ya Bunge litakaloundwa kutokana na baadhi ya wajumbe kutaka mambo ya Tanzania Bara yajadiliwe na Watanzania Bara tu na pia yawepo mambo ya Muungano ambayo yatajadiliwa na wabunge kutoka pande zote za Muungano.

Hoja ya uraia pacha pamoja na suala la Kadhi Mkuu nalo ni miongoni mwa yanayodaiwa kukabiliwa na mvutano ndani ya baadhi ya kamati.
Source:Habari Leo

No comments:

Post a Comment