Friday, August 1, 2014

Wasailiwa 6740 kujaza nafasi 47 TBS


TAASISI na idara za Serikali zimeendelea na utaratibu mbovu wa kuajiri kwa kuita wasailiwa wengi kwa nafasi chache walizotangaza, ulioasisiwa na Idara ya Uhamiaji. Jana Shirika la Viwango Tanzania (TBS), lilianza kuwafanyia usaili watu 6,740 kwa ajili ya kuwania nafasi 47 tu zilizowazi, zilizotangazwa Aprili mwaka huu.

Wakati Idara ya Uhamiaji ililazimika kufanya usaili wa watu zaidi ya 10,000 katika Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kujaza nafasi 70 tu, TBS wao wameamua kufanya usaili kwa siku mbili katika Ukumbi wa Yombo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Usaili huo tofauti na ule wa Idara ya Uhamiaji ambapo wasailiwa walifanya kwa wakati mmoja, kwa TBS usaili ulifanyika kwa saa moja na nusu kwa kila nafasi.
Gazeti hili lilitembelea katika eneo hilo la usaili na kukuta wasailiwa wakifika na vyeti vyao halisi, ambavyo walivionesha katika meza ya kwanza kwa ajili ya kujisajili na baadaye kusubiri kuingia katika chumba cha kufanyia usaili.
 Mara baada ya kufika katika chumba hicho cha usaili walikaguliwa vitambulisho na vyeti tayari kwa ajili ya kufanya usaili huo wa maandishi, uliosimamiwa na maofisa mbalimbali wa Wizara ya Kazi na Ajira pamoja na Wizara ya Utumishi.
Ofisa mmoja wa TBS, ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema usaili huo unafanywa kwa usimamizi wa taasisi mbalimbali za Serikali na TBS hawahusiki kabisa.
Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya wasailiwa hao, walidai wamefika hapo kwa ajili ya kupata uzoefu wa usaili na wanaamini kilichotokea katika nafasi za kazi za Idara ya Uhamiaji kitatokea na hapo.
Walisema baada ya kuona idadi ya watu walioitwa katika usaili na nafasi zilizopo, walikata tamaa na kueleza bayana kuwa ni vema kukawa na utaratibu mwingine wa kuwaita ili
kuwafanya wasikate tamaa kabla ya usaili.
Mmoja wa wasailiwa (jina limehifadhiwa),aliyefika hapo kwa ajili ya usaili wa nafasi ya Mtaalamu wa Kompyuta, alisema wamefika wasailiwa 300 wakati nafasi iliyo wazi ni moja, jambo
ambalo linashangaza ni vipi watawachuja na kupata mmoja bila upendeleo.
Mwingine (jina limehifadhiwa), ambaye alifika kufanya usaili wa nafasi ya Mhasibu Msaidizi, alisema kuitwa watu wengi kunasaidia kupata uzoefu kwa ajili ya kazi nyingine lakini nivigumu kupata nafasi hizo.
Alisema katika nafasi hiyo ya Mhasibu Msaidizi, wanaohitajika ni watu watatu lakini walioitwa ni watu 700 jambo ambalo limewafanya wengi kukata tama.
Msailiwa mmoja wa nafasi ya Ofisa Rasilimali Watu, ambaye alifanya kazi katika taasisi isiyo ya kiserikali
 na amemaliza muda wake nchini, alisema ni vema katika kutangaza nafasi wasitoe za jumla wawe na sifa wanazotaka
Alisema kuita watu wengi kiasi hicho kunatia shaka na kuonesha kuna jambo linaendelea, kwani katika nafasi hiyo kunahitajika watu watatu, lakini wameitwa zaidi ya watu 870 jambo linalofanya waone itakuwa vigumu kutenda haki kwa watu wote hao
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko, alisema ili kuepuka kuchaguliwa kwa waombaji wenye uhusiano na wafanyakazi wa shirika hilo, kazi hiyo ya usaili inafanywa na taasisi
 nyingine na TBS itapelekewa majina 47 ya watakaokuwa wamekidhi vigezo
Masikitiko alisema katika nia hiyo hiyo ya kuepuka upendeleo, wameamua kujivua kusimamia mchakato huo na utafanywa na taasisi mbalimbali, ikiwemo Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) kwa lengo la kuepuka yale yaliyotokea katika Idara ya Uhamiaji.
Alisema kati ya nafasi za kazi 22 zilizotangazwa, nafasi iliyoombwa na watu wachache ni ya Ofisa Maabara Msaidizi ambayo imeombwa na watu 61 na anatakiwa mtu mmoja.
Alisema katika nafasi ya Mhasibu Msaidizi, wameomba watu 1,360, lakini wanaotakiwa kuajiriwa ni watu watatu tu.

Source:Habari Leo

No comments:

Post a Comment