
KUMEKUCHA katika Bunge Maalumu la Katiba, ambapo sasa baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamekiuka viapo na vitisho vya viongozi wao, kwa kuamua kutinga bungeni.
Katika
mijadala mbalimbali, msemaji wa Ukawa ambaye pia ni Mwanasheria wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu,amekuwa akisisitiza kwamba
wajumbe wa Ukawa na hasa kutoka Chadema, hawatahudhuria Bunge Maalumu la Katiba.
Aidha,
wiki iliyopita Chama cha Wananchi (CUF) kilisambaza waraka kwa vyombo vya
habari, kuwataka wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotoka katika chama
hicho, kutohudhuria vikao vya Bunge hilo, vilivyoanza juzi.
Hata
hivyo, katika kile kilichoonesha kutoungwa mkono kwa viongozi wa Ukawa ndani ya
vyama vyao, baadhi ya wabunge waliozuiwa kushiriki vikao hivyo, wameonekana
bungeni wakijisajili, kuashiria ushiriki wao bila kujali viapo na makatazo ya
viongozi wao
Leticia,
ShibudaJana
saa 5:55 asubuhi mjumbe wa bunge hilo, Leticia Nyerere ambaye ni
Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Chadema,
aliwasili kwenye viwanja vya bunge na kwenda moja kwa moja kwenye eneo la
kujisajili na kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
Hata
hivyo, Leticia hakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari, wakati akienda kujiandikisha.
Hata
wakati anatoka kukamilisha taratibu zinazotakiwa za kujisajili, pia alikataa
kupigwa picha. “Unajua kwamba kunipiga picha bila idhini yangu ni ‘illegal
(kinyume na sheria)? Sitaki,” alisema huku akielekea
mlango
wa kutokea, ambako alikutana na mjumbe mwingine wa bunge hilo, ambaye pia ni
Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani (CCM), aliyekuwa akitoka pia
kujisajili.
Ngonyani
alisalimiana na Leticia na wakawa wanaongozana kutoka eneo
la
Bunge. Ngonyani alionekana mwenye furaha baada ya mjumbe mwenzake,
kukamilisha
taratibu za usajili.
Mapema
juzi, wajumbe wengine wa Bunge hilo, Mbunge wa Maswa Mashariki, John Shibuda
(Chadema) na Clara Mwatuka ambaye ni Mjumbe wa Viti Maalum kutoka CUF, nao
walijisajili kushiriki vikao hivyo.
Wanaojishauri.
Jana
asubuhi pia zilikuwepo taarifa bungeni kwamba Mbunge wa Mpanda Kati, Said Arfi
(Chadema), naye alijisajili. Lakini, akizungumza na gazeti hili kwa simu,
alisema alifika Dodoma, lakini hajaamua kama
ajisajili
ili ashiriki vikao au la
“Sijajisajili
bado, sio kweli, sijaamua nichukue huo uamuzi wa kushiriki au la, kama nikitaka
kujisajili nitasema, ila kweli nipo
Dodoma,”
alisema Arfi ambaye alijiuzulu nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa
Taifa
wa Chadema hivi karibuni.
Zitto
Mbunge
wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), hivi karibuni aliibuka na kupingana
na harakati za Ukawa.
Zitto
alikaririwa akisema, hana uhakika wala hauamini Ukawa kama
utakuwa
umoja endelevu hadi kufikia Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, kwa sababu
si mara ya kwanza vyama vya upinzani, kuungana
na kugawanyika.
Zitto
alitoa kauli hiyo wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Power Breakfast,
kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds cha jijini Dar es Salaam, ambapo
alisema Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi na si Katiba pekee.
Alisema
siku zote Watanzania, wamekuwa wakipenda kuwa na upinzani imara, ambao watu
wanaweka tofauti zao pembeni na kuungana dhidi ya chama ambacho kinaongoza,
lakini haoni kama Ukawa utaendelea hadi kufikia kipindi cha Uchaguzi Mkuu.
Alisema
hatua ya kusimama kwenye ajenda moja ya Katiba, haitausaidia umoja huo, kwani
kipindi cha Uchaguzi Mkuu, kinakuwa na ajenda nyingi.
Alisema wananchi watapenda kusikia masuala ya
kushughulikia rushwa, matumizi ya rasilimali, maji, umeme, afya na barabara.
“Mambo
haya ndiyo yatakayowafanya wananchi waamue namna gani watakabidhi dhamana ya
uongozi, si suala la Katiba pekee,” alisema Zitto.
Sitta
Juzi wakati akizungumza bungeni, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alisema
zaidi ya robo tatu ya wajumbe wa bunge hilo, walikuwa wamejiandikisha, ingawa
hakutaja namba kamili. Pia, majina ya
waliojiandikisha,
hayatolewi kwa vyombo vya habari.
Kwa
mujibu wa Sitta, wajumbe wakishajisajli, fedha zao zinawekwa kwenye akaunti zao
moja kwa moja kwa wale wenye akaunti ya Benki ya NMB.
Wale ambao hawana akaunti NMB, wanachukua
mkononi.
Aidha,
katika mitandao mbalimbali, kulikuwa na taarifa kuwa karibu wajumbe 50 kutoka
Ukawa, walikuwa wameshafika Dodoma, ingawa
hawakuonekana
katika viwanja vya Bunge.
Taarifa
zingine zilieleza kuwa katika vyama hivyo, baadhi ya wabunge wanalalamikia
viongozi wao, kususia Bunge Maalumu kutokana na ajenda zao binafsi, huku wao
wakitakiwa na wapiga kura wao kuhudhuria bunge hilo.
Wajumbe
waliojiundia kundi la Ukawa ambao wanatoka vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na
CUF walisusia vikao vya bunge hilo Aprili mwaka huu,kwa kile walichodai
halijadili Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya
Jaji Joseph Warioba.
Bulembo
Wakati huohuo, Mjumbe wa Bunge hilo, Alhaji Abdallah Bulembo,alisema anaamini
Katiba itapatikana na Ukawa watazidi kupasuka kadri
muda
unavyoenda.
“Tayari
wameanza kujiandikisha, nasema watagawanyika siku si nyingi na Katiba
itapatikana, hotuba ya Mwenyekiti (Sitta) juzi ilikuwa nzuri
sana
na imetoa mwelekeo wa mzuri,” alisema Bulembo, ambaye anatoka Kundi la Wajumbe
201, walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
“Leo
(jana) tumeanza kujadili rasimu kwenye kamati, tunajadili bila jazba, tunaenda
vizuri na naamini mambo yatakamilika kama tunvyopanga.
Gazeti
hili lilimtafuta Msemaji wa CUF, lakini mara zote simu yake haikupatikana.
Baadaye,
gazeti hili lilimpigia simu Jusa Ismail na kumuuliza juu ya tukio la Mbunge wa
CUF, Clara Mwatuka kujisajili katika Bunge Maalum la Katiba, linaloendelea na
vikao vyake huko Dodoma.
Jusa
alijibu, “Siwezi kukisemea Chama. Mimi ni Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama,
naomba umtafute Naibu Katibu Mkuu wa chama, Magdalena Sakaya, atakupa
ufafanuzi”.
Ndipo,
gazeti lilimpigia simu Sakaya, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum wa CUF.
Lakini, mara zote simu yake ilikuwa haipatikani.
Kwa
upande wa Chadema, gazeti hili lilimpigia simu Mkurugenzi wa Uenezi wa Chadema,
John Mnyika ili atoe ufafanuzi wa juu wa wabunge wao wawili, Leticia Nyerere na
John Shibuda, kujisajili kwenye Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma.
Hata
hivyo, simu zote mbili za Mnyika, hazikupatikana hadi tunakwenda mtamboni.
Source:Habari
Leo
No comments:
Post a Comment