Jeraha la mgongoni alilopata Flora Porokwa.
MKE wa Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za
Wafugaji la Pingos Forum, Edward Porokwa, Flora Porokwa (37), mkazi wa Sakina
Kwaidi amepigwa risasi na watu wanaohisiwa kuwa ni majambazi.
Tukio hilo lilitokea juzikati ambapo risasi hiyo
alipigwa kwapani na kwenda kutokea mgongoni na kulazimika kuendesha gari umbali
wa kilometa moja akiwa na risasi mwilini.
Majeruhi huyo ambaye amelazwa katika Hospitali
ya Seliani jijini hapa, alionesha ujasiri wa hali ya juu baada ya kumudu
kuendesha gari hilo huku watu hao wawili waliokuwa wamepanda bodaboda
wakiendelea kumfuatilia hadi alipofika nje ya nyumba yake ambapo aliishiwa
nguvu na kupoteza fahamu akiwa anasubiri kufunguliwa geti la kuingia ndani.
Akizungumza kwa tabu hospitalini hapo, majeruhi huyo
alisema tukio hilo lilimtokea jioni ya saa moja kasoro katika Barabara ya
Arusha - Namanga eneo la Kwaidi ambapo watu hao walimvamia ghafla na kulizuia
gari lake kwa mbele wakitumia pikipiki hiyo.
Alisema mmoja wa watu hao alimfuata na kushika
kitasa cha mlango wa mbele na kujaribu kufungua lakini mlango haukufunguka. Ndipo
mwanamke huyo alipoamua kushusha kioo cha mlango ili aweze kumsikiliza, lakini
ghafla jambazi huyo alichomoa bastola na kumpiga risasi kwapani.
“Kwenye gari sikuwa na fedha, sijui kama walilenga
kunipora au kuna tatizo lingine. Nikiwaona naweza kuwakumbuka kwa sura ila
siwajui, sikuwahi kuwaona kabla,’’ alisema mwanamke huyo na kuongeza kuwa:
“Namshukuru Mungu kwa kuniepusha na kifo kwani
dhamira yao ilikuwa kuniua.”
Majeruhi huyo ambaye hali yake bado siyo vizuri, alitoa rai kwa jeshi la polisi mkoani Arusha kuwasaka watu hao kisha kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Hadi sasa tukio hilo halijafahamika undani wake kama
watu hao walilenga kupora fedha au ni kisasi, kwani kabla ya tukio hilo
kuna taarifa kwamba hata mumewe, Porokwa aliwahi kupigwa risasi na watu
wasiojulikana.
Jirani mmoja wa mama huyo ambaye hakupenda jina lake
liandikwe gazetini, alisema wamesikitishwa mno na tukio la mwenzao kupigwa
risasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas hakupatikana kuzungumzia tukio hilo.
No comments:
Post a Comment