VITENDO vya
baadhi ya wazazi, kudhalilisha walimu vinaendelea, ambapo mzazi mmoja Selemani
Juma, amewashambulia walimu wawili kwa viboko.
Amefanya
hivyo kupinga mwanawe kurudishwa nyumbani, akashone kaptura. Alifanya hivyo
mwishoni mwa wiki iliyopita.
Taarifa
zilizofikia gazeti hili zilibainisha kuwa Juma alidhalilisha walimu wawili wa Shule ya Msingi Nzogimlole
iliyopo wilayani Nzega mkoani Tabora.
Aliwashambulia kwa viboko, akipinga kitendo cha mwalimu mmojawapo, kumrudisha
nyumbani mwanawe.
Gazeti
hili lilifika katika shule hiyo, yenye walimu tisa tu na kuzungumza na Mwalimu Mkuu Msaidizi, Emmanuel
Josephat, ambaye alisema mwanafunzi huyo, Shaaban Maziku anayesoma darasa la
pili, alipeleka ujumbe tofauti na
alioagizwa na walimu kwa baba yake, hivyo kusababisha
kadhia
hiyo.
Kwa
mujibu wa Mwalimu Josephat, mwalimu aliyedhalilishwa (jina limehifadhiwa),
alikuwa akifundisha katika darasa hilo na alipomuona mwanafunzi huyo kavaa kaptura iliyochanika
vibaya, kiasi cha sehemu za siri kuonekana, alimrudisha nyumbani kwenda
kurekebisha sare yake.
Mwalimu
Josephat alisema mwalimu huyo wa kiume wa darasa la pili, alimwagiza mwanafunzi
wake aende kwa baba yake, akamuombe amsaidie kushona kaptura hiyo.
‘’Mwalimu
hana kosa, kwani mtoto kaptura yake ilikuwa imechanika vibaya kiasi cha sehemu zake za siri
kuonekana… walimu hatupaswi tuwaache hivi watoto, mwalimu alichofanya ni
kumwambia akamwambie baba yake aishone ile sare, lakini mambo hayakuwa hivyo,’’
alisema Mwalimu Josephat.
Akizungumza
kwa majonzi, Mwalimu Josephat alisema mtoto huyo alipofika nyumbani, alimweleza baba yake kuwa
mwalimu huyo, amechana kaptura hiyo na
amemwagiza arudi nyumbani kwenda kumwambia baba huyo aishone.
Ujumbe
huo unadaiwa kusababisha mzazi huyo, kufika shuleni na kuanza kutoa lugha chafu dhidi ya mwalimu huyo na
baadaye baba huyo alianza kutoa kipigo.
Mwalimu
Josephat alidai kuwa baba huyo, alianza kutumia mawe kurusha kwa walimu hao.
Baadaye alitumia fimbo, kumchapa mwalimu huyo wa darasa la pili.
Hatua
hiyo inadaiwa ilisababisha mwalimu huyo, kupiga mayowe kuomba msaada. Wananafunzi waliokuwa darasani,
walitoka na kuanza kumsaidia kupiga
kelele za kuomba msaada.
Mayowe
hayo yalisaidia mwalimu mwenzake, Elias Kafiku kutoka ofisini kwa nia ya kuamua
ugomvi huo ili wazungumze kiofisi na kufikia
muafaka.Lakini, mwalimu huyo pia aliambulia kipigo.
Kutokana
na kipigo hicho, mwalimu huyo wa darasa la pili alipata majeraha na kupelekwa
zahanati ya kijiji, ambako alipatiwa huduma na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Akizungumza
na gazeti hili, mwalimu huyo wa darasa la pili alisema hali yake inaendelea
vizuri. Alisema sababu ya kupigwa na mzazi huyo, hazijui kwa kuwa alitekeleza
majukumu yake kama kawaida.
Akitoa
maoni yake kuhusu tukio hilo, Mwalimu Elizabeth Kafulila wa shule hiyo, alisema
tukio hilo limewatia hofu katika utendaji kazi, kutokana na mzazi kuingilia
majukumu ya walimu.
Mwalimu
Elizabeth aliwataka wazazi kujirekebisha na kushirikiana na walimu katika kulea watoto wao, na wanapokuwa
na malalamiko, wafuate taratibu za kiofisi.
Kamanda
wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda alisema mzazi huyo anashikiliwa kwa
tuhuma za kupiga na kujeruhi vibaya na atafikishwa mahakamani baada ya
upelelezi kukamilika
No comments:
Post a Comment