
KAMATI
nyingi za Bunge Maalumu la Katiba, zimekataa sifa ya elimu ya kidato cha nne,
kuwa kigezo cha msingi cha mgombea ubunge, kwa madai kuwa inabagua wananchi kwa
kuondoa haki yao ya kidemokrasia ya kuomba kupigiwa kura na kupiga kura.
Hata
hivyo, kamati hizo zimeweka sifa ya kuwa mbunge, iwe ni kujua kusoma na
kuandika, bila kufafanua kama sifa hiyo nayo, inaweza kuleta ubaguzi huo.
Ibara
ya 26 kifungu cha kwanza cha rasimu ya Katiba, kinaeleza kuwa sifa ya kugombea
ubunge ni kujua kusoma na kuandika, lugha ya Kiswahili na Kiingeza na ana elimu
isiyopungua kidato cha nne.
Lakini
taarifa za kamati nyingi zimeeleza kuwa suala la kugombea nafasi yoyote ni la
kidemokrasia, haipaswi mtu kuzuiwa kugombea kwa kigezo cha elimu, kwani hii ni
haki ya kikatiba.
Katiba
haitakiwi kuweka kigezo chochote kinachokiuka haki za msingi za kuchaguliwa au
kuchagua,” ilisema taarifa namba 10 ya Bunge hilo. Kamati hiyo pia ilisema haki
ya kuamua kama mgombea anafaa au hafai ni ya wapiga kura, wasizuiwe kikatiba
kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua mtu wanayemtaka.
Walisema
utaratibu huo haupo duniani kote hata nchi zilizokomaa na demokrasia
iliyokomaa.
Ni
kamati namba mbili tu, ndio ambayo imetaka sifa ya mtu kuwa mbunge iwe elimu ya
kidato cha nne, lakini pia awe ni raia wa kuzaliwa na hana uraia wa nchi
nyingine na aliyetimiza umri wa miaka 21.
Kuhusu
watu ambao waliwahi kukutwa na makosa ya jinai kutogombea, baadhi ya kamati
zinapendekeza kuwa makosa hayo yawe ya ubakaji au ujangili, ili kutowakataza
waliohukumiwa kwa makosa madogo madogo ya jinai na kunyimwa fursa ya kugombea
nafasi ya ubunge.
Wajumbe
hao pia wametaka ibara ya pili (a) inayozungumzia muda wa ukomo wa ubunge wa
vipindi vitatu, ifutwe ili kuwapa fursa wabunge ambao ni watendaji wazuri
katika maeneo yao, kuendelea kugombea na kuchaguliwa na wananchi kwa sababu
kimsingi ni haki ya mtu kikatiba.
Pia
walisema hiyo itawapa uhuru wananchi kuchagua mbunge wanayemtaka, hata kama
ameshashika madaraka hayo kwa vipindi vitatu mfululizo.
Hata
hivyo wametofautiana katika eneo la watumishi wa umma wanapoamua kugombea
ubunge, urais na udiwani makamu wa rais au nafasi nyingine katika chama cha
siasa, wapo wanataka mtu huyo utumishi wake ukome pale anapogombea, lakini wapo
wanaotaka mtumishi huyo ahesabiwe kama yuko likizo bila malipo.
Kwa
upande wa uongozi wa Bunge, karibia kamati zote zimekubaliana na rasimu ya Tume
ya Marekebisho ya Katiba ambayo yanataka mbunge, waziri, naibu waziri
wasiruhusiwe kugombea uspika wala unaibu uspika.
Sababu
za kukubaliana na hoja hiyo ni kwamba ni kutoa uhuru kwa spika na naibu wake
kufanya kazi yake kwa uhuru bila kuingiliwa na chama chake cha siasa.
No comments:
Post a Comment