MADAKTARI
bingwa wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, masikio na viungo kutoka
nchini Misri wako nchini. Wamekuja kufanya kampeni maalumu ya afya, upasuaji na
huduma mbalimbali kwa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na Kitengo
cha Mifupa Muhimbili (MOI.
Chini
ya kampeni hiyo, wagonjwa walioidhinishwa kufanyiwa upasuaji katika maeneo
hayo, watapatiwa huduma na madaktari hao hadi Jumatatu ijayo.
Walianza
kutoa huduma jana. Huduma ya upasuaji kwa madaktari hao, imeandaliwa na Shirika
la Kimataifa linalojihusisha na utoaji wa misaada na huduma kwa jamii ya
Al-Rahma International na African Relief Committee of Kuwait kwa kushirikiana
na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza
jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Othman Kiloloma alisema
Tanzania ina upungufu mkubwa wa madaktari bingwa wa maeneo hayo, hususani
ubongo na mishipa ya fahamu, ambapo kwa sasa wako watano.
“Licha
ya upungufu wa madaktari wa maeneo hayo lakini waliopo wako MOI jambo ambalo
husababisha kutofikiwa kwa wagonjwa wengi na ambao wana mahitaji ya haraka
hususani wale walioko maeneo ya pembezoni,” alisema Dk Kiloloma.
Aliongeza
kuwa wataalamu wengi, bado wako masomoni nchini Misri na Afrika Kusini.
Alisema
kwa viwango vinavyotakiwa, daktari bingwa wa mishipa ya fahamu na ubongo,
hutakiwa kuwaona wagonjwa 6,000 lakini kutokana na uhaba wa madaktari daktari
mmoja hujikuta akiona wagonjwa milioni 11 hadi 12.
Akizungumza
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Masikio, Profesa Mohammed el Begermy alisema
wamekuja nchini kwa lengo la kuokoa wagonjwa wa masikio, ambao wengine wamejikuta
wakishindwa kusikia.
Alisema
wana uwezo wa kufanya upasuaji, utakaowezesha mgonjwa kusikia tena, kwani
asilimia 60 ya wagonjwa wasiosikia hukutana na hali hiyo kutokana na kushindwa
kufikiwa na huduma stahiki, huku watoto wengine wakishindwa kutamka maneno kwa
kushindwa kusikia.
Kwa
upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu, Profesa
Hussein Moharram alisema eneo hilo ni la kipekee ambalo huchukua muda mrefu
kusomea na linahitaji kutoa huduma kubwa na za dharura.
“Kupata
mtaalamu wa eneo hili, inahitajika kusoma takribani miaka 10 hadi 15 na
kutokana na wanaosomea taaluma hiyo kutafuta njia ya mkato, hivyo husababisha
wataalamu wa eneo hilo kuwa wachache kwani hata upasuaji wake huchukua muda
mrefu kuanzia saa sita,” alisema.
Alisema
kuwepo katika kampeni hiyo, kutasaidia kushirikiana na wataalamu wa Tanzania,
kuongeza uzoefu na kuharakisha huduma kwa wagonjwa.
No comments:
Post a Comment