Kumekuwepo na madai yanayosambazwa kupitia njia mbalimbali za
upashanaji habari kuhusu baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) kuonekana mjini Dodoma au kujisajili kwa ajili ya kuhudhuria vikao
vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini humo.
Chama
kupitia Idara ya Habari kingependa kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo;
1. Uamuzi
wa kuwataka wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wanaotokana na CHADEMA
kushirikiana na wenzao wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA),
kutoshiriki vikao vya bunge hilo ili kuepuka kunajisi mchakato wa Katiba Mpya,
ulitokana na maazimio ya kikao cha Kamati Kuu iliyoketi Julai 18-19 na kuazimia
kwamba;
§ Wajumbe wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA,
kama sehemu ya UKAWA, watarudi kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu mamlaka
ya Bunge hilo yatafafanuliwa kuwa ni ya kuboresha, na sio kuibomoa au kuifuta,
misingi mikuu (basic features) ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na maoni ya
wananchi na kuandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoteuliwa na Rais kwa
ajili hiyo;
§ Wajumbe wa Bunge Maalum wanaotokana na CHADEMA,
kama sehemu ya UKAWA, watarudi kwenye vikao vya Bunge Maalum endapo tu, na
baada ya, ufafanuzi uliotajwa katika aya ya 2 utahusisha marekebisho ya kifungu
cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, inayohusu mamlaka ya
Bunge Maalum, pamoja na Kanuni husika za Bunge Maalum;
§ Wajumbe wote wa CHADEMA katika Bunge Maalum
hawatashiriki katika kikao chochote cha Bunge Maalum au Kamati zake hadi hapo
ufafanuzi wa mamlaka ya Bunge Maalum uliotajwa katika aya za 2 na 3
utakapofanyika kwa mujibu wa maazimjo ya Kamati Kuu;
Hadi
wakati huu, hakuna jambo hata moja kati ya hayo lililofanyika, huku mazungumzo
yaliyotarajiwa kuokoa mchakato yakiwa yamevunjika, kwa sababu CCM na Serikali
yake wameamua kudharau na kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo kwenye Rasimu ya
Katiba badala yake kuweka maslahi ya chama hicho kwenye katiba.
2. Iwapo kuna mjumbe/wajumbe wa Bunge
Maalum la Katiba wanaotokana na CHADEMA wameonekana wakijisajili kwa ajili ya
kuhudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma au
watashiriki vikao vya bunge hilo au kamati zake, wataandikiwa barua ya
kujieleza kisha chama kitachukua hatua kwa mujibu wa taratibu zake kupitia
vikao.
3. Tunapenda pia kuwakumbusha
wanachama wa CHADEMA na umma mkubwa wa Watanzania kuwa, mji wa Dodoma mbali ya
kuwa Makao Makuu ya Nchi pia inapatikana Ofisi Kuu ya Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Kuendelea
kwa Bunge Maalum la Katiba ambako hakujaridhiwa na Watanzania wengi, hakujazuia
shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanyika ikiwemo kutoa
huduma kwa watu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wabunge. Suala hilo linakwenda
sambamba na ukweli kwamba sehemu kubwa ya watumishi wa Bunge Maalum la Katiba
ni wale wale ambao wanatakiwa kuwahudumia wabunge wa Bunge Maalum la Katiba.
Hivyo
kuonekana kwa mbunge yeyote wa CHADEMA mjini Dodoma au kwenye viwanja au Ofisi
za Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuwezi kutafsiriwa moja kwa moja
kuwa mbunge husika amehudhuria vikao vya Bunge Maalum la Katiba, kinyume na
msimamo wa UKAWA.
Imetolewa
leo Alhamis Agosti 7, 2014 na;
Tumaini
Makene
Mkuu
wa Idara ya Habari- CHADEMA
No comments:
Post a Comment