Thursday, July 24, 2014

Waliotupa viungo vya binadamu kushughulikiwa kikamilifu




Tukio la utupaji wa viungo vya binadamu jalalani, linalodaiwa kufanywa  Chuo cha Kimataifa cha Matibabu na Teknolojia (IMTU) cha Dar es Salaam, linadaiwa kuandika historia mbaya nchini.
Wakati  serikali ikiendelea kuchunguza tukio hilo, ikiwemo kuunda tume nyingine chini ya Wizara ya Afya na Ustawi, kujiridhisha kabla ya hatua
kuchukuliwa,Baraza la Madaktari limetwishwa mzigo wa kuhakikisha  linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na kitendo hicho Serikali  imetumia nafasi hiyo kuonya vyuo vingine, kwa kusema  jambo hili ni la kusikitisha, la aina yake katika historia ya mafunzo ya udaktari
tangu yaanze nchini takribani miaka 40 sasa.
"Pia  tunatoa onyo kwa vyuo vingine, mafunzo haya tumeanza miaka 40 iliyopita lakini haijawahi kutokea kitu cha aina hii, ni mara ya kwanza ni jambo  la kusikitisha sana," alisema Naibu Waziri wa Wizara ya Afya na Ustawi, Dk Steven Kebwe
Naibu Waziri aliwaambia waandishi wa habari kuwa kitendo hicho cha kutupa
viungo vya binadamu hadharani, si jambo la kawaida, ni la uvunjifu wa haki za kibinadamu.
Katika kile kinachodhihirisha chuo hicho kung’ang’aniwa, kabla ya kuamua hatua
 za kuchukua dhidi yake, Wizara hiyo yenye dhamana ya afya, pia imeunda  kamati ya watu 15 kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo.Kamati  hiyo ya wizara iliyopewa siku saba kukamilisha kazi, imeundwa kukiwa na tume nyingine iliyoundwa na Polisi Kanda ya Dar es Salaam, kuchunguza
sakata hilo la kutupwa viungo katika maeneo ya Bonde la Mbweni Mpiji, Bunju jijini Dar es Salaam.
Dk Kebwe aliwaambia waandishi wa habari kwamba kamati hiyo ya wizara itafanya kazi yake kwa siku saba kuanzia juzi. Inajumuisha wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu, Polisi na Wizara ya Afya na Ustawi.
Aidha, alisema zipo sheria zinazoelekeza namna ya kuteketeza miili hiyo baada ya kumalizika kwa kazi yake.
“Lakini inasikitisha kuona miili hiyo ilitelekezwa na watu wanaojua maadili ya kazi ya udaktari,” alisema.
Alisema  kwa kuwa madaktari huwa wanakula viapo baada ya kumaliza mafunzo yao,
Baraza la Madaktari nchini linatakiwa kuhakikisha linachukua hatua kali kwa watakaobainika kuhusika na kitendo hicho.
Timu iliyoundwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imejielekeza kuja na majibu kadhaa,ikiwa ni pamoja na kufahamu idadi kamili ya watu wenye viungo hivyo.Ikiwa na watu saba akiwemo.Mkemia Mkuu wa Serikali, itakuja na majibu yanayofafanua viungo hivyo ni vya muda gani na zilitumika kemikali gani kuvikausha.
 

No comments:

Post a Comment