Tuesday, July 22, 2014

NEWS:WATUHUMIWA WA MABOMU ARUSHA, HAWA HAPA.



MKE na mume, wakazi wa Sombetini jijini Arusha wanatuhumiwa kukutwa
na mabomu saba ya kutupa kwa mkono aina ya grumeti , unga wa baruti,
risasi vikihusishwa na matukio ya ulipuaji mabomu jijini hapa.
Wakati wanandoa hao, Yusuph Ally (30) na mkewe, Sumaiya Juma (19),
wakishikiliwa na Polisi, pia watu sita akiwemo mwalimu wa shule ya
msingi, walinzi watatu na mfanyabiashara, wanashikiliwa kwa tuhuma za
kuhusika katika ulipuaji wa mghahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine,
 jijini hapa.
Kuhusu wanandoa hao wanaotuhumiwa kukutwa na silaha hizo, Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Issaya Mngulu alisema
walikamatwa juzi usiku nyumbani kwao.
 Mngulu alisema polisi katika mwendelezo wa kusaka watuhumiwa wa
ulipuaji mabomu, inashikilia watu hao kupata taarifa zaidi ni wapi
mabomu hayo yametoka.
Mngulu ambaye alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari jijini
 hapa, alisema moja kati ya mabomu yaliyokamatwa, kwa mujibu wa
wataalamu, limetoka Ujerumani na yaliyobaki yametengenezwa Urusi.
“Bado tunawashikilia watu hawa ambao ni mke na mume ili kujua mabomu
haya walikuwa nayo ni ya nini. Pia bado tunafuatilia watu wengine
wanaohusika na ulipuaji wa mabomu na nasema hivi hatutaishia hapa
tutaendelea na upelelezi wetu hadi kieleweke,’’ alisema Mngulu.
Kwa mujibu wa Mngulu, mtuhumiwa Yusuph (mume), ni miongoni mwa
waliokuwa wakitafutwa kwa tuhuma za ulipuaji wa mabomu jijini Arusha.
 Alisema mtandao wa wanaohusika na mabomu ni mkubwa, huku watu zaidi
ya 25 wakiendelea kutafutwa na wengine 25 wanashikiliwa na Polisi. Muda
wowote watafikishwa mahakamani.
Ulipuaji mgahawa Wakati huo huo, Mngulu ametaja watu sita
wanaotuhumiwa kuhusika katika ulipuaji wa mgahawa wa Vama Traditional
Indian Cuisine. Katika mlipuko huo wa hivi karibuni, watu wanane
wakiwemo wanne wa familia moja, walijeruhiwa.
Watuhumiwa hao ni aliyekuwa mlinzi wa mgahawa huo, Shaban Mmasa (26)
na Athuman Mmasa (38) ambaye ni mlinzi wa mgahawa wa Chinese uliopo
Gymkhana, jirani na Vama Traditional Indian Cuisine.
 Wengine ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Olturnet, Jaffar Lema (38)
ambaye alikuwa Imam wa Msikiti wa Quba mjini Arusha. Mwalimu huyo
anatuhumiwa miongoni mwa viongozi walioratibu matukio ya mabomu maeneo
mbalimbali.
Watuhumiwa wengine ni Abdul Salim (31) ambaye ni wakala wa mabasi
jijini Arusha, mfanyabiashara Said Temba (42) mlinzi wa mgahawa wa
Chinese, Mohamed Nuru (30).
Katika hatua nyingine, Polisi imesema inamtafuta Yahaya Hella (35),
mkazi wa Mianzini, akituhumiwa kuhusika na ulipuaji wa mabomu nchini.
Anadaiwa kuwa mtaalamu wa kung fu.
Hata hivyo, DCI alikanusha kuwa baadhi ya watuhumiwa wanaokamatwa
wanahusishwa na mgogoro wa Msikiti wa Masjid Quba. Alisisitiza kukamatwa
 kwa watuhumiwa hao hakuhusiani na masuala ya imani
Source:Habari Leo

No comments:

Post a Comment